Chuo cha DON BOSCO Dodoma chaanza kutoa kozi ya kilimo cha kisasa cha Umwagiliaji

Chuo chetu cha DON BOSCO kwa kushirikiana na ubalozi wa Israel

Chuo cha Ufundi Stadi cha DON BOSCO kilichopo jijini Dodoma kwa kushirikiana na ubalozi wa Israel hapa nchini na wadau mbalimbali kimeanza kutoa kozi ya kilimo cha kisasa kitakachoweza kuzalisha wataalamu wa kilimo cha kisasa cha umwagiliaji.

 

Akizungumza kwenye uzinduzi wa kozi hiyo mpya katika chuo hicho Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge ameitaka jamii kuchangamkia fulsa hiyo kwani ni fulsa mpya kabisa hapa nchini kupata kozi ya kilimo cha kisasa katika elimu kazi ya kati.

“Tukio hili ni muhimu sana hasa katika Mkoa wa Dodoma, mwanzo tulizoea kuona kozi za kilimo zilikuwa zikitolewa ngazi ya chuo kikuu ni niwachache waliokuwa na uwezo wa kufikia huko, lakini sasa DONBOSCO wameanza kutoa kozi hii ni fulsa kubwa wananchi waichangamkie hasa katika kilimo cha mboga mboga” amesema Dkt Mahenge.

Amesema kitendo cha nchi ya Israel kuleta wataalamu wa kufundisha kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia teknolojia ni fulsa kwani hapo mwanzo tulikuwa tukipeleka wataalamu nchini Israel kwenda kusoma pia waliokuwa wakipata nafasi ya kwenda kusoma walikuwa wachache lakini sasa wataalamu wamekuja hapa nchini ni fulsa kubwa.

“Israel wao wamepiga hatua kubwa sana katika kilimo hasa cha umwagiliaji na mifugo kwahiyo wataalamu kuwapata hapa nchini ni fulsa kubwa sana, mwanzo waliokuwa wanapata nafasi walikuwa wachache kama nchi tulikuwa tunaweza kupeleka watu wa tano, lakini sasa kupitia DONBOSCO watapata fulsa hiyo wengi zaidi” amesema.

Amewataka wataalamu watakaopata elimu ya kilimo katika chuo hicho kwenda kuwa walimu kwa wengine huko vijijini katika jamii inayowazunguka hasa kupata elimu ya umwagiliaji kwa kutumia matone ambayo inapunguza upotevu wa maji hasa katika maeneo yenye upungufu wa maji ambapo wanaweza kuvuna maji ya mvua na kuyatumia katika kilimo hicho.

Ameongeza kuwa “tumepita katika lile shamba darasa naona hamjiamini kabisa katika katika kutoa mlivyofundishwa, ukifundishwa kit una ukakifahamu jitahidi kujiamini katika kuelezea unachokifahamu, hawa walimu wanaowafundisha wao wamepiga hatua kubwa katika kilimo kwahiyo wanajua” amesema.

- Ad Keep reading below -

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha DON BOSCO Padri. Boniface Mchami, amesema chuo hicho kipo katika usajili wa VETA na kimekuwa kikitoa kozi mbalimbali ikiwamo ufundi bomba, uselemala, ufundi magari, kuchomelea vipuli, kushona, upishi na nyingine nyingi.

 

Amesema kwa sasa kwa kushirikiana ubalozi wa Israel, kupitia mradi wa CultAid na shirika la Innovation for Afrika na water for Mercy wameanzisha kozi mpya ya kufundisha kilimo cha kisasa kinachotumia maji machache na mfumo unaosoma kiwango cha maji yanayozalishwa na maji yanayotumika katika umwagiliaji shambani.

Amesema kozi hiyo itakuwa ya miezi nane 8 ambapo miezi 6 wataitumia kusoma darasani na miezi miwili wataitumia kufanya mazoezi kwa vitendo katika maeneo tofauti, huku akibainisha kuwa chuo kina shamba darasa lenye ukubwa wa ekari 6 yenye miondombinu yote ya kufundishia kama kisima, mfumo wa umeme na bwawa la kutunzia maji kabla ya kusukumwa kwenda shabani.

Nae Meneja mradi wa Innovetion Afrika Bi. Lerian Mosha amesema walianza shughuli zao hapa nchini mwaka 2006 katika utekelezaji wa miradi ya huduma za kijamii maeneo ya vijijini ambako mara nyingi hawapati fulsa kama hizo katika maji safi na umeme wa jua ambapo walianza katika Mkoa wa Pwani na sasa Dodoma.

Amesema kupitia mradi huo wamejiunga na chuo cha DON BOSCO ili kupitia utekelezaji wao waweze kusaidia teknolojia yao ya mfumo wa maji na umeme wa jua katika kutoa maji kisimani na kuyasukuma kwenda shambani kupitia mifumo hiyo.